UNIVERSITY OF PENNSYLVANIA - AFRICAN STUDIES CENTER
IRIN-CEA: Taarifa ya Wiki ya IRIN 19-98 kwa kipindi cha 1-7 Mei 1998

IRIN-CEA: Taarifa ya Wiki ya IRIN 19-98 kwa kipindi cha 1-7 Mei 1998

U M O J A W A M A T A I F A Ofisi inayosimamia masilahi ya kibinadamu IRIN kwa Afrika ya Kati na ya Mashariki

Tel: +254 2 622 147 Fax: +254 2 622 129 e-mail: irin@ocha.unon.org

IRIN-CEA: Taarifa ya Wiki ya IRIN 19-98 kwa kipindi cha 1-7 Mei 1998

[Muhtasari wa kila wiki umetokana na habari za kila siku zilizoletwa IRIN na maelezo mengine muhimu kutoka kwa mashirika ya Umoja Wa Mataifa, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Serikali mbalimbali, wahisani na vyombo vya habari. IRIN inatoa ripoti hizi kwa manufaa ya jamii inayoangalia maslahi ya kibinadamu, lakini haikubali kuwajibika kuhusika kwenye usahihi wa habari wa aliyezileta/huko zilikotoka.]

RWANDA: Annan alaumu ukosefu wa nia ya kisiasa kwenye mauaji ya kinyama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, ameweka lawama ya kushindwa kuzuia mauaji ya kinyama ya 1994 kwenye "ukosefu wa nia ya kisiasa" na sio kukosa kutaarifiwa. Kushindwa huku kumetokana na "wenyeji, taifa na jamii ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na nchi wanachama zenye uwezo; ni lawama kwetu sote", aliambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Nairobi siku ya Jumatatu. Annan alikuwa akijibu madai yaliyoandikwa na gazeti la 'New Yorker' la tarehe 3 Mei, yaliyodai kwamba DPKO, ambayo yeye Annan mwenyewe alikuwa akiiongoza wakati huo, mwanzoni, ilipuuza tahadhari zilizokuwa zimetolewa kuhusu mauaji ambayo yangetokea hapo baadaye. "Hakuna anayeweza kukana kwamba dunia haikutimiza wajibu wake kwa watu wa Rwanda. Lakini swala muhimu leo sio kuangalia nyuma na kutafuta nani atupiwe lawama. Inatubidi tujiulize tufanye nini unyama kama huo usitokee tena, na jinsi gani jamii ya kimataifa yaweza kusaidia watu na serikali ya Rwanda katika kazi kubwa ya kulijenga taifa lenye umoja na kuwasahaulisha yaliyopita", Annan alisema hayo pia kwenye taarifa aliyotoa huko Nairobi.

Dallaire aamriwa asiingilie kati - 'New Yorker'

Kwenye nakala lake la mwisho, gazeti la 'New Yorker' lilisema Annan, baada ya kupokea fax kutoka kwa Jenerali Romeo Dallaire aliyomtumia tarehe 11 Januari 1994, Annan aliamuru kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani kisiingilie kati. Dallaire, mzaliwa wa Canada, ndiye aliyekuwa muu wa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani huko Rwanda. Dallaire alikuwa amepata ripoti kutoka kwa jasusi wa ngazi ya juu wa serikali ya Rwanda aliyekuwa ameamriwa kuandika orodha ya Watutsi waliokuwa wakiishi mji mkuu wa Kigali. Jasusi huyo, ambaye alikuwa mmoja wa wapambe wa aliyekuwa rais wa Rwanda, Juvenal Habyrimana, alisema watu wake "wangeweza kuua Watutsi elfu moja" kwa dakika 20, fax hiyo ilisema. Alijitolea kukisaidia kikosi cha Umoja wa Mataifa kuvamia sehemu zilizofichwa silaha za wanamgambo wa Kihutu. Naye Dallaire alifahamisha makao makuu ya Umoja wa Mataifa kwamba alinuia kuvamia sehemu hizo kwenya muda wa masaa 36 baadaye. DPKO ilijibu kwamba kulingana na uwezo na kanuni walizopewa wasingeweza kufanya kazi hiyo, na ikashauri Dallaire aende kumwarifu Habyarimana habari hizo.

Annan alisema kwamba Katibu Mkuu aliyemtangulia, Boutros Boutros-Ghali, alisukuma sana nchi wanachama waipatie "Umoja wa Mataifa nguvu, nyezo za kufanya kitu Rwanda" lakini hakufaulu. Annan alisema anakubaliana na maoni ya Dallaire kwamba kama kikosi kingepewa nguvu zaidi maisha ya "mamia ya maelfu" yasingepotea.

Annan asifu kazi ya mahakama ya Arusha

Annan amefika Arusha siku ya Jumanne, na akasifu "maendeleo" yaliyofanywa na Mahakama ya Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Rwanda (ICTR) katika utendaji kazi wake. "Ninajivunia maendeleo mliyofanya kwenye utendaji kazi wa mahakama kwa mwaka mmoja uliopita", Annan alisema. Siku ya Jumatatu, Annan alisema kuwa mapendekezo ya kutaka ICTR ihamishiwe Nairobi ni "tetesi" tu.

Aliyekuwa afisa wa serikali atiwa nguvuni kuhusiana na mauaji ya kinyama

Serikali ya Rwanda imemkamata aliyekuwa afisa wa serikali kuhusiana na mauaji ya 1994. Redio Rwanda ilitangaza kwamba imechukua zaidi ya miaka miwili ya uchunguzi kabla ya aliyekuwa "directeur de cabinet" katika ofisi ya Waziri Mkuu, Antoine Bizimana, kutiwa nguvuni. Alitiwa nguvuni huko nyumbani kwake Mbazi, wilaya ya Butare, kufuatilia "ushahidi usiokanika" wa kwake kuhusika kwenye mauaji hayo ya kinyama. Kiongozi wa mashtaka wa Butare, Martin Ngoga, alisema kusikilizwa kwa kesi ya Bizimana kutaanza kabla ya wiki mbili kumalizika.

Mvua kubwa zasabibisha barabara kufungwa

WFP ilisema kwenye ripoti yake ya wiki ya hivi majuzi kwamba mvua kubwa na mafuriko vimesababisha sehemu za barabara kuu mbili kufungwa. Matope yamefunga barabara inayounganisha Butare na Cyangugu na sehemu ingine ya barabara inayounganisha Kigali na Gisenyi imebomoka kabisa hivyo kulazimisha magari kubadilisha njia.

Idadi ya wakimbizi kufikia zaidi ya 34,000

Katika ripoti yake, WFP imesema, idadi ya wakimbizi Rwanda kwa sasa imefikia 34,710. Kati ya hawa Wakongo 31,771 wamewekwa kwenye makambi huko Byumba na Kibuye na Waburundi 2,939 wanakaa kwenye makambi matatu huko Cyangugu, Butare na Gikongoro. Idadi ya Wakongo inaendelea kuongezeka, ili hali Waburundi wanarudi manyumbani mwao kidogo kidogo. WFP imesema kuwa pia Waburundi kutoka kambi za Kibondo, Tanzania, wanarudi makwao kwa hiari yao.

ICTR yampata na hatia ya mauaji ya kinyama aliyekuwa Waziri Mkuu Ikitoa hukumu yake ya kwanza, Mahakama ya Kimataifa inayashughulikia Rwanda (ICTR), siku ya Ijumaa, ilimpata na hatia aliyekuwa Waziri Mkuu wa Rwanda, Jean Kambanda, kwenye mashtaka sita ya mauaji ya kinyama na makosa dhidi ya ubinadamu, baada ya yeye mwenyewe kuyakiri makosa yote. Hukumu itatolewa siku itakayotangazwa baadaye. Kukiri kwake huku kutaruhusu Kambanda kuwa mshahidi mkuu wa upande wa mashtaka kwenye makesi mengine. Wakati huo huo, watuhumiwa 15 wa mauaji ya kinyama waliofungiwa kwenye gereza kuu la Kigali, wamekiri kuhusika kwao kwenye uchinjaji huo na wakaomba wasamehewe, redio Rwanda ilitangaza.

Msaidizi wa kiongozi wa mashtaka, Bernard Muna, aliambia mkutano wa waandishi wa habari kwamba Kambanda atakuwa tayari kutoa ushahidi kwenye makesi mengine mbele ya Mahakama ya Umoja wa Mataifa, shirika la habari la kujitegemea la Hirondelle, liliripoti. "Alisema kwamba kama akiombwa kutoa ushahidi wa yaliyotokea na anayoyajua, hatasita kufanya hivyo", Muna alisema. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, alieleza kuwa kukiri huko na kupatikana huko na hatia ni "hatua ya maan a sana".

Serikali ya Rwanda yasifu kukiri kwa makosa

Serikali ya Rwanda imesifu kitendo cha kukiri makosa, lakini ikasema si ajabu hata kidogo. "Si jambo la kushangaza kwamba Kambanda amekiri mashtaka", Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, Anastase Gasana, aliliambia shirika la habari la Rwanda (RNA). Alisema Kambanda alijua vizuri sana uzito uliopo wa ushahidi dhidi yake. "Ingekuwa ni jambo zuri sana kama angetoboa mambo yote anayoyajua juu ya mpango wa mauaji ya kinyama, waliohusika, na jinsi ulivyotekelezwa nchini kote", Gasana aliongeza kusema. Wakati huo huo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limekubali kupanua mahakama ya kimataifa inayosikiliza makesi ya mauaji ya kinyama ya 1994 ya Rwanda katika juhudi zake za huharakisha uchunguzi. Taarifa ya habar i ilisema baraza hilo, Alhamisi iliyopita, liliafikiana kwa pamoja azimio la kuanzisha chumba cha tatu cha kuzikilizia makesi.

BURUNDI: ACF yafungua kituo cha kulisha waliodhoofika sana huko Bubanza

Shirika lisilo la kiserikali, 'Action contre la faim' (ACF), limefungua kituo cha kwanza cha kulisha waliodhoofika sana huko mji mkuu wa mkoa, Bubanza. Kituo hiki kinaweza kuhudumia watu 750, mjumbe wa ACF aliambia IRIN. Uchunguzi wa lishe uliofanywa na 'Children's Aid Direct' (CAD), ulionyesha kwamba zaidi ya watoto 2,000 waliopokelewa kwenye mpango wa kusaidia kulisha katika mkoa huo walihitaji lishe hii maalum. Uchunguzi huo ulikazia kwamba ukosefu wa chakula bora ndio uliosababisha vifo vingi, na ukasema kila siku kati ya watoto 10,000 wenye umri kotoka miezi 6 hadi miezi 59, aslimia 4.34 wanakufa. CAD ilisema ina mpango wa kufungua kituo kingine cha kusaidia kulisha huko Musigati, kuongezea vile sita vilivyoko kwenye mkoa. Watakaofaidika na vituo hivi ni watu 5,700, wengi wao wakiwa ni watoto. Wakati huo huo, OCHA huko Burundi imeripoti kwamba idadi ya watu wanaoishi kwenye makambi huko mkoa wa Bubanza hivi majuzi imeongezeka kufikia 159,000 mwezi Aprili. Hii ina maana kwamba asilimia 57 ya watu wa mkoa h uu sasa wanaishi kwenye makambi, msemaji wa maslahi ya kibinadamu alisema.

Serikali ya Burundi imekanusha uwepo wa vifo vingi makambini

Serikali ya Burundi imekanusha vikali madai ya vyombo vya habari kwamba kuna vifo vingi vinavyotokea kwenye makambi ya watu waliokimbia makwao. Kwenye mahojiano na shirika la habari la Rwanda, Waziri wa Mawasiliano, Pierre Claver Ndayicariye, alieleza kuwa taarifa hiyo ni "uwongo mtupu na ina nia mbaya". "Habari hizi za uwongo zinatoka kwa watu ambao wanaonea wivu maendeleo ya serikali yetu", alisema. Aliongezea, idadi iliyotolewa na IDPs ya watu 500,000 "ilitiliwa chumvi sana", akisema watu wengi wameshapewa makao tayari. Wafungwa waachiliwa huru kwa sababu ya msongamano

Zaidi ya wafungwa 80 wameachiliwa huru kutoka magereza ya Mpimba huko Bujumbura kwa sababu ya msongamano kwenye magereza ya nchi hiyo. Kulingana na habari za shirika la habari la All Africa, walioachiliwa huru si wale waliohukumiwa na makosa ya uuaji, ufujaji wa mali ya umma, wizi wa kutumia silaha au ulaji rushwa. Habari z a mahakama zasema watu 9,000 wamefungwa kwenye magereza ya Burundi ambayo yaweza kupokea tu watu 3,650. Mpimba ina wafungwa 2,544 wakati uwezo wake ni wa wafungwa 800 tu. Zaidi ya msongamano magereza yanazidi kushindwa kulisha wafungwa kwa sababu ya ongezeko la bei za mazao ya shamba, shirika hilo lilisema.

UGANDA: Taasisi zafungwa kuzuia kuenea kwa kipindupindu

Wizara ya Afya imeamuru kufungwa kwa baadhi ya taasisi huko kaskazini mwa wilaya ya Arua, afisa wa ngazi ya juu wa wizara, Sam Okura, aliambia IRIN. Alisema, kikundi kilichoteuliwa kushughulikia kipindupindu kimefunga "taasisi zisizozingatia usafi kama mashule na masoko". Watu watano wamekufa na 18 wako hospitalini tangu kipindupindu kilipozuka kwenye eneo hilo wiki mbili zilizopita. Wakati huo huo maambukizi ya kipindupindu kwenye eneo la Bundibugyo yameongezeka kukiwa na vifo 16 vilivyoripotiwa kwenye makambi ya watu waliotoroka makwao ya Itojo na Karugutu, WFP ilisema. Mashirika ya kutoa misaada yanajaribu kupambana na hali hiyo.

Waasi waua wanane Kasese

AFP imeliripoti jeshi kama likisema kwamba siku ya Alhamisi waasi waliwaua watu wanane wakati wa mashambulizi huko wilaya ya Kasese, magharibi ya Uganda. Waasi wa Allied Democratic Forces (ADF) walimkatakata vipande maiti ya mtu mmoja baada ya kumuua. Mwanamke mmoja aliyeponea mauaji hayo baada ya kufungiwa kwa muda mfupi na waasi, aliliambia gazeti la kujitegemea 'Monitor' kwamba aliona waasi kama 30 hivi waliobeba silaha kali waliokuwa wamevaa mavazi ya kipolisi na kijeshi. Kamanda wa ngazi ya juu wa jeshi, ambaye aliomba asitajwe, aliambia AFP kwamba waasi hao walikuwa na nia ya kuvizia magari kwenye barabara ya Bwera-Lake Katwe, lakini wakabadilisha mawazo walipoona malori ya jeshi yakishika doria.

CONGO-BRAZZAVILLE: UNICEF kufungua kituo cha watoto waliodhurika akili kwa vita

UNICEF imeanzisha kituo huko Brazzaville cha kutoa matibabu ya akili kwa maelfu ya watoto waliodhurika akili kwa sababu ya vita huko Jamhuri ya Congo. Mpango kama huo wa UNICEF huko Rwanda bado unaendelea kutoa huduma ya ushauri kwa watoto wanaoumia kutokana na kilema cha shinikizo baada ya kudhurika kwenye mauaji ya kinyama ya 1994, na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea. Reuters ilimnukuu msemaji Patrick McCormick akisema karibu watoto wote 450,000 chini ya miaka 18 mjini Brazzaville waliviona vitendo vya kudhurisha akili wakati wa vita vya Congo vya miezi minne vilivyotokea mwaka jana.

SUDAN: Mazungumzo ya amani yaisha kwa makubaliano ya kujiamulia mambo yao

Mazungumzo ya amani kati ya serikali ya Sudan na waasi wa SPLA, yamemalizika jana hapa Nairobi yakiahidi kuitisha kura ya maoni huko Sudan ya kusini juu ya uwezo wa kujiamulia mambo yao wenyewe. Kwenye taarifa iliyosomwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Bonaya Godana, alisema mazungumzo yaliyo chini ya usimamizi wa IGAD yamepiga hatua, ijapokuwa hayakuweza kufikia makubaliano kuhusu serikali na dini. Redio Kenya ilitangaza kuwa pande zote mbili zimekubali usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwenye sehemu za nchi zilizoathiriwa "uwe huru na usiwe na vizuizi". Walikubaliana kukutana tena huko Addis Ababa baada ya miezi mitatu.

WFP yatangaza kuongeza kwa safari za ndege

WFP imetangaza kuanzishwa kwa safari ya ndege ya ziada aina ya C-130 ambayo ilianza kuangushia vyakula watu 50,000 wanaoishi kusini mwa Sudan kwenye miji ya Ajak na Akon katika jimbo la Bahr al-Ghazal. Katika taarifa yake, WFP, ilisema utekelezaji huo ni baada ya serikali ya Sudan kukubali siku ya Jumapili iliyopita Umoja wa Mataifa kutumia ndege tatu zaidi aina ya C-130, hivyo kufanya idadi ya ndege zote kuwa tano. Msimamizi wa WFP wa Sekta ya Kusini, David Fletcher, alieleza kwamba ndege hizi zitasidia kuokoa maisha ya maelfu ya Wasudan. Wanaotoa huduma za misaada wamesema ndege hizi zinafika kwa wakati unaofaa. OLS, sekta ya kusini, inasema ina uhakika wa kukabiliana vilivyo na utoaji wa dharura unaohitajika sana kwa vile Khartoum imetoa vibali vipya vya kutumia ndege kubwa na kuwaongezea maeneo ya huduma. Msemaji wa OLS alisema kwamba shida kubwa sasa ni kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kutekeleza.

TANZANIA: Saba wafa kwa mafuriko

Mkuu wa polisi wa mkoa wa Dar es Salaam, Alfred Gewe, aliambia IRIN siku ya Jumatano Kwamba watu saba walizama na wengine 1,000 kukosa makao wakati mafuriko yaliikumba Dar es Salaam baada ya mvua kubwa iliyonyesha huko Jumapili na Jumatatu. Habari nyingine zasema watu 70 walikufa baada ya basi walimokuwa wakisafiria kutumbukia kwenye mto uliokuwa umefurika huko mkoa wa Tanga, 'Daily Nation' iliripoti Jumatatu. Dereva alishindwa kuliona daraja "lililokuwa limefunikwa na maji ya mafuriko" kwa sababu ya mvua za masika zinazoendelea.

JAMHURI YA KIDEMOKRASIA YA CONGO (DRC): Olenghankoy atiwa mbaroni tena, asema waziri

Waziri wa Ndani wa DRC, Gaetan Kakudji, siku ya Ijumaa alitangaza kwenye televisheni ya serikali kwamba mwanasiasa wa upinzani, Joseph Olenghankoy, ambaye alikuwa ametoroka kwenye gereza lenye ulinzi mkali huko Buluwo, jimbo la Katanga, amekamatwa tena. Inasemekana Olenghankoy alishikiwa kijiji cha Tenke, kilichoko umbali wa kilometa 80 kutoka gereza la Buluwo, na askari wa usalama, na kwa sasa atafungiwa huko Lubumbashi, waziri alisema. Olenghankoy, rais wa chama cha FONUS (Forces novatices pour l'union et la solarite) alitoroka akiwa pamoja na waf ungwa wengine maarufu ambao walikamatwa baadaye na kuonyeshwa kwenye televisheni wiki iliyopita.

Habari nyingine ziliripotiwa na shirika la habari la PANA zasema kwamba zaidi ya waandishi wa habari 10 wameshatiwa nguvuni tangu tarehe 17 Mei, wakati Rais Laurent-Desire Kabila alipotwaa mamlaka. Likinukuu vyombo vya habari huko Kinshasa, shirika lilisema, kwenye makala ambayo iliandikwa kuambatana na Siku ya Uhuru wa Magazeti Duniani, Jumapili iliyopita, kwamba kutiwa nguvuni huko kulifanyika kwa sababu tatu - kuandika habari za uhasama kuhusu serikali iliyo mamlakani, kuunga mkono upinzani na kile serikali inachokiita "kujiingiza kwenya hisia za adui". Adhabu zilizotolewa kwa waliotiwa nguvuni ni pamoja na kuhojiwa kwa masaa mengi kwa wengine na wengine kufungiwa gerezani kwa miezi mitatu kwenye "kituo cha serikali cha kuelimisha tena" (Penitentiary Reeducation Centre) kilichoko gereza la zamani la Makala.

Serikali yasisitiza kurudi kwa waliokuwa maafisa wa Mobutu

Serikali ya DRC imetoa mwito kwa nchi za nje ambazo zinawapa hifadhi waliokuwa maafisa wa Serikali ya Mobutu Sese Seko, wawarudishe Kinshasa. Kwenye taarifa iliyosomwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Bizima Karaha, kwenye televisheni ya DRC, ilisema maisha yao hayatakuwa hatarini, na uchangiaji wao katika kuijenga upya nchi hiyo unahitajika.

Mkutano wa Maziwa Makuu waandaliwa

Serikali ya DRC inaandaa mkutano wa eneo la Maziwa Makuu huko Kinshasa utakaofanyika kuanzia tarehe 12 Mei hadi 16 Mei. Viongozi wa nchi za Burundi, Ethiopia, Kenya, Uganda, Rwanda, Tanzania na Zambia wamealikwa kwenye mkutano huo ambao una malengo ya kutafuta amani na utulivu katika eneo na kuzindua mwanzo wa maendeleo kieneo. Tarehe 17 Mei kutakuwa na maadhimisho ya mwaka mmoja tangu serikali ya Rais Laurent-Desire Kabila kuingia mamlakani. Wachunguzi wanasema baadhi ya nchi na mabalozi wanaowakilisha nchi zao DRC wanaweza kususia mkutano huo wakihofia kuwa ni njia ya serikali hiyo kuhakikisha kushiriki kwa watu wengi kwenye maadhimisho ya mwaka mmoja ya kusherehekea kuondolewa mamlakani kwa dikteta Mobutu Sese Seko.

ANGOLA: Hali ya usalama yazorota

Hali ya Usalama ya Angola yasemekana imezorota kufuatilia mzozano ulioripotiwa kati ya askari wa usalama na maharamia - ambao ni mabaki ya UNITA. Msemaji mmoja wa wa kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa, MONUA, aliambia IRIN kwamba kwenye majimbo ya Benguela, Malange, Huila na Uige "hali ni mbaya sana" kiasi cha wanakijiji kutoroka mzozano huo mkali. Televisheni ya serikali ya Angola, siku ya Jumanne, ilisema hali ya kijeshi ya jimbo la kusini la Benguela "imefikia kiwango cha vita". Wasemaji wa maslahi ya kibinadamu wanasema mapigano yanaendelea kati ya polisi na "ambao wanadhaniwa kuwa maharamia" katika tarafa nne za mkoa huo.

Nairobi, 8 Mei 1998, 11:00 GMT

[MWISHO]

[Habari zilizoko kwenye jarida hili zinakujia kwa kupitia IRIN, Idara ya Umoja wa Mataifa inayotoa maelezo/habari ya maswala ya kibinadamu, lakini si lazima kwamba hayo ndiyo maoni ya Umoja wa Mataifa au mashirika yake, Kwa maelezo zaidi au kwa kujisajili na jarida hili tuma kwa UN IRIN Simu: +254 2 622123. Fax: +254 2 622129. E-mail: irin@ocha.unon.org Endapo utalipiga tena chapa jarida hili, kulinukuu, kulihifadhi kwa kumbukumbu au kulituma tena kwa njia ya posta, tafadhali onyesha kutohusika kwenye uhakika wa taarifa. Unukuaji wa maneno au ibara lazima u onyeshe ni kwa mujibu wa mahali habari zilikotoka. Ripoti za IRIN zinahifadhiwa kwa kumbukumbu katika WWW kwenye <http://www.reliefweb.int/emergenc> au zinaweza kupatikana mara moja kwa kutuma e-mail kwenye anuani archive@ocha.unon.org. Mailing list: irin-cea-swahili-wiki.]

Date: Mon, 11 May 1998 18:13:00 -0300 (GMT+3) From: Ben Parker <ben@ocha.unon.org> Subject: IRIN-CEA: Taarifa ya Wiki ya IRIN 19-98 kwa kipindi cha 1-7 Mei 1998 Message-ID: <Pine.LNX.3.95.980511181137.9846G-100000@amahoro.dha.unon.org>

Editor: Dr. Ali B. Ali-Dinar, Ph.D

Previous Menu Home Page What's New Search Country Specific